Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linamshikilia Musa Bashiri Mushi (40), mkazi wa KDC, Kata ya Mbokomu, Wilaya ya Moshi Mjini , akituhumiwa kuwatapeli fedha watalii kupitia mtandao.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro Simon Maigwa amesema mtuhumiwa huyo kwa nyakati tofauti amekuwa akitumia mitandao ya kijamii kufungua akaunti zinazojinasibisha na biashara ya utalii, kisha kufanya udanganyifu kwa kuwaibia fedha wageni wanaopanga au wanaoingia nchini kwa shughuli za utalii.
Amesema baada ya kupokelewa kwa taarifa za tukio hilo katika Kituo cha Polisi Moshi Kati, askari waliweka mtego maalumu uliofanikisha kumkamata mtuhumiwa huyo juzi.
Amesema uchunguzi zaidi unaendelea, ikiwa ni pamoja na kukusanya ushahidi, ili hatua nyingine za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yake.
Ametoa wito kwa wananchi na raia wa kigeni ambao wamewahi kutapeliwa na mtuhumiwa huyo, kufika polisi ili kusaidia kukamilisha uchunguzi na kuchukuliwa kwa hatua za kisheria.
Chanzo; Nipashe