Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kinondoni imetangaza kuwasaka Alex Msama Mwita na Benny Mwita Sammoh wanaokabiliwa na shauri la uhujumu uchumi namba 1371/2026 katika Mahakama ya Kisutu. Watuhumiwa hao wanatuhumiwa kwa makosa mazito ikiwemo kuongoza genge la uhalifu, kughushi hati za ardhi, na kujipatia zaidi ya shilingi milioni 984 kwa njia ya udanganyifu kupitia uuzaji haramu wa kiwanja kilichopo eneo la Vijibweni, Kigamboni.
Uchunguzi uliotekelezwa na timu ya TAKUKURU Kinondoni na Temeke umebaini kuwa washtakiwa walighushi hati ya mauziano ya kiwanja namba 33 mali ya kampuni ya Africa Energy Limited na kukiuzia kampuni ya World Oil Tanzania Limited kwa mkataba wa shilingi bilioni 1.7. Katika mchakato huo, Benny Mwita anadaiwa kutumia jina la bandia la Ben Samson na baadaye kumhamishia Alex Msama kiasi cha shilingi milioni 370 kama sehemu ya mapato ya udanganyifu huo.
Licha ya kutakiwa kuripoti ofisi za TAKUKURU tangu Desemba 2025, watuhumiwa hao wamekaidi amri hiyo na kutokomea kusikojulikana, jambo lililopelekea Mahakama ya Kisutu kutoa hati ya kuwakamata tarehe 21 Januari 2026. Aidha, Alex Msama anatafutwa pia kwa tuhuma nyingine za kughushi na kuvamia kiwanja eneo la Regent Estate Mikocheni, huku taasisi hiyo ikiahidi kutoa zawadi nono kwa mwananchi yeyote atakayefanikisha kupatikana kwao.
TAKUKURU imetoa tahadhari kwa watumishi wa umma kutoshiriki katika udanganyifu wa milki za ardhi na kuwataka wananchi kuwa makini na kufanya uhakiki wa kina kabla ya kununua viwanja, hususan katika maeneo ya kimkakati. Wananchi wamehimizwa kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa kupitia namba 0738 150236, ikisisitizwa kuwa kuzuia rushwa ni jukumu la kila mmoja ili kulinda haki na rasilimali za Taifa.
hanzo; Itv