Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa ameagiza hospitali zote nchini kuanza mara moja utekelezaji wa katazo la kuzuia maiti kwa sababu ya madeni ya matibabu, akisisitiza kuwa agizo hilo ni la lazima na halitakiwi kukaidiwa.
Amesema hakuna Mtanzania atakayenyimwa huduma ya matibabu kwa kukosa fedha wala familia kunyimwa mwili wa mpendwa wao, akibainisha kuwa vitendo vya kuzuia maiti vinakiuka utu na maadili ya Taifa.
Mchengerwa amezitaka hospitali kutafuta vyanzo mbadala vya mapato badala ya kuwaumiza wananchi, akionya kuwa viongozi watakaokiuka agizo hilo watachukuliwa hatua za kisheria na kinidhamu.
Ametoa agizo hilo leo Desemba 8, 2025 alipokuwa akizungumza kwenye kikao kazi na watumishi wa sekta ya afya kilichofanyika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), akisisitiza kuwa utekelezaji wake utafuatiliwa kikamilifu katika hospitali zote za umma na binafsi.
“Wizara itaendelea kufanya ukaguzi wa kushtukiza kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa haki, staha na ulinzi wa utu wao hata baada ya kifo,”amesisitiza Mchengerwa.
Chanzo; Mwananchi