Raia wa Ghana, Valentine Kofi (45) na Watanzania watatu, wataendelea kubaki rumande hadi Desemba 15, 2025 wakati kesi yao ya uhujumu uchumi itakapotajwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Hatua hiyo inatokana na upelelezi wa kesi hiyo kutokamilika.
Kofi na wenzake wanakabiliwa na mashtaka manne likiwemo la kuingilia mfumo wa benki na kuiba Sh2 bilioni, mali ya benki ya Banc ABC.
Leo Jumatatu Desemba Mosi, 2025, Wakili wa Serikali Roida Mwakamele, amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini, kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea na wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Hakimu Mhini amekubaliana na ombi la upande wa mashtaka na kuahirisha kesi hiyo hadi Desemba 15, 2025 kwa kujatwa.
Washtakiwa wamerudishwa rumande kutoka na shtaka la kutakatisha fedha linalomkabili halina dhamana kwa mujibu wa sheria.
Mbali na Kofi ambaye ni mkazi ya Mikocheni washtakiwa wengine ni Patrick Tarimo (34) mkazi wa Kibaha, Aisha Kagashe (40) mkazi wa Sinza na Idan Msuya (46) mkazi wa Mikocheni.
Chanzo; Mwananchi