Search

Saved articles

You have not yet added any article to your bookmarks!

Browse articles

GDPR Compliance

We use cookies to ensure you get the best experience on our website. By continuing to use our site, you accept our use of cookies, Privacy Policy, and Terms of Service.

Hofu ya Machafuko Tanzania Yazua Ununuzi wa Dharula

Msongamano mkubwa wa wananchi umeshuhudiwa hivi karibuni katika masoko na maduka makubwa nchini Tanzania, huku wakazi wakinunua chakula, maji, na bidhaa nyingine muhimu kwa wingi.

Ripoti kutoka vyombo vya habari vya ndani, ikiwemo gazeti la The Citizen, zimeripoti foleni ndefu katika maduka jijini Dar es Salaam, ambako watu wameonekana wakijaza toroli na bidhaa muhimu za nyumbani.

Hali hii ya ununuzi wa dharura imehusishwa moja kwa moja na hofu ya kufanyika maandamano mengine ambayo yamepigwa marufuku na Jeshi la Polisi tarehe 9 Disemba.

Wakati baadhi ya wananchi wanajitayarisha kwa hofu ya kukosekana kwa bidhaa, wengine wanasema ni tahadhari ya kudhibiti hatari zinazoweza kutokea kutokana na machafuko ya kisiasa.

Wachambuzi wa masuala ya kijamii wanasema hali hiyo inaonyesha jinsi wananchi wanavyoweza kuhofia matokeo ya kisiasa na kuibua tabia ya "kujikinga mapema."

BBC imezungumza na baadhi ya wakazi wa jijini Dar es Salaam na Mbeya ambapo, maandamano na vurugu zake zilileta athari kubwa ambazo serikali inaendelea kutathimini kupitia Tume ya uchunguzi iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

"Sijui hali itakavyokuwa siku hiyo. Nimeona ni vyema kununua mapema mahitaji yangu ili nisitoke nyumbani kuepuka usumbufu iwapo kutatokea maandamano," alisema Inviolatha, mkazi wa Kijichi jijini Dar es Salaam.

Katika mikoa mingine, tahadhari kama hiyo imeonekana pia. "Hapa Mbeya tulipata athari za tukio la Oktoba 29. Sitaki kukaa bila bidhaa za msingi," alisema Tatu Kajembe, mkazi wa Mbeya.

Baadhi ya wakazi pia wameeleza wasiwasi wa kupanda kwa bei za bidhaa na nyingine kuadimika.

"Nimefanya manunuzi kuhofia Kutopata huduma kutokana na hofu ya maandamano, sehemu nyingi za kutolea huduma zinakuwa zimefungwa au bidhaaa kupanda bei kiholela" anasema mkazi mwingine wa jijini Dar es Salaam, Bernad Shaban.

Ruth Kimath, mkazi mwingine wa jijini humo, alisema: "Nilikwenda soko la Mabibo, tayari baadhi ya bidhaa hazikupatikana, na hali hiyo haikuwa kawaida wiki zilizopita." Kuna baadhi ya bidhaa kama za nafaka, pia viazi, mihogo, magimbi bei imepanda jana mpaka 3000- 4000Tsh kwa fungu katika baadhi ya maeneo jijini Dar es Salaam.

Hali hii inajiri huku askari polisi na wanajeshi wakionekana kwa wingi wakishika doria katika maeneo kadhaa ya nchi. Serikali imehimiza utulivu na kuimarisha ulinzi, huku Jeshi la Polisi likisisitiza kuwa maandamano hayo yanahatarisha amani na usalama wa raia.

Kundi la vijana linaendelea kuhamasisha maandamano ya Disemba 9, licha ya marufuku, wakidai kutoridhika na mwenendo wa matukio ya kisiasa nchini, wakidai katiba mpya, mabadiliko ya mifumo ya kisiasa, hoja ambazo Serikali inasema zimefanyiwa kazi na zingine hasa ya katiba iko kwenye ilani ya CCM, na itafanyiwa kazi.

Maandamano ya Oktoba 29 yalisababisha vifo na uharibifu wa mali za umma na binafsi, jambo lililochochea serikali kuongeza ulinzi na kufuatilia kwa karibu shughuli za wanasiasa na wanaharakati.

Wiki iliyopita, Rais Samia aliwahakikishia wazee wa Dar es Salaam kuwa serikali "imejipanga" kukabiliana na hali yoyote itakayojitokeza. "Likija wakati wowote, tumejipanga," alisema, akiongeza: "Tutasimama na kuilinda nchi hii kwa nguvu zote."

Kauli hii inaashiria kuwa mamlaka zipo makini katika kuhakikisha usalama wa raia na mali zao, lakini pia inaonyesha namna serikali inavyochukulia hofu ya wananchi kwa uzito na kutaka kuhakikisha usalama wao na kuendelea kwa shughuli kawaida.

Wakati wa maandamano na ghasia za Oktoba 29, karibu siku tatu mpaka tano watu walikaa ndani jijini Dar es Salaam na kusumbuka kupata huduma muhimu. Pengine ununuzi wa dharura wa sasa ni kujiandaa kama itatokea hali kama hiyo tena.

 

Chanzo; Dw

Kuhusiana na mada hii: