Eneo la Chanika Mwisho maarufu Chanika Mjini ambalo huwa na pilikapilika nyingi za kibiashara na usafiri wa daladala leo Jumanne Desemba 9, 2025 lina utulivu usio wa kawaida.
Mwananchi limepita maeneo hayo ambayo hadi saa 6:00 mchana yamekuwa na ulinzi wa askari wa Jeshi la Polisi, na kukiwa na vizuizi pande zote za kuingia na kutoka huku wananchi wakilalamikia kuadimika mikate.
Askari hao sambamba na wale wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) baadhi wana silaha za moto na wengine wana fimbo mkononi.
Imeshuhudiwa madumu, matenga ya nyanya na meza za wafanyabiashara vikiwa vimefungwa kamba na kutumika kama vizuizi barabarani.
Vizuizi hivyo vimewekwa barabara ya kuingia na kutokea Homboza, wilayani Kisarawe, mkoani Pwani.
Vingine vimewekwa barabara ya kuelekea Mvuti, Mbagala na ile inayoelekea Katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
Katika vizuizi hivyo, wanaopita wamekuwa wakionyesha vitambulisho, huku wale ambao hawakuwa navyo wanatakiwa kurudi walikotoka.
Chanzo; Mwananchi