Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba ametoa maagizo kwa viongozi wa majiji na halmashauri zote nchini kuhakikisha wafanyabiashara hawanyang’anywi bidhaa zao na badala yake wawaelekeze namna bora ya kufuata taratibu zilizowekwa.
“…Msichukue bidhaa za raia; hizo ndio ofisi za raia wetu, hata kama kuna jambo ambalo anapaswa kuelekezwa kuhusu masuala ya utaratibu basi mshughulikie jambo linalohusu utaratibu, msizuie mitaji ya watu. Utaratibu wa kuchukua bidhaa haukubaliki na hakuna uhalali wa kuchukua bidhaa za raia. Msicheze na mitaji ya watu.”
Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo (Jumatatu, Desemba 8, 2025) wakati akizungumza na wafanyabiashara katika soko la Machinga jijini Dodoma baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa Richard Joseph ambaye ni mfanyabiashara sokoni hapo aliyedai kuchukuliwa bidhaa zake na watumishi wa jiji.
Mheshimiwa Dkt Mwigulu amemuagiza mkuu wa mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule pamoja na Mkuu wa wilaya ya Dodoma Jabir Shekimweri wahakikishe wanafuatilia suala hilo na wahusika warudishe bidhaa za mfanyabiashara. “Kama wamepotea nazo, wachukuliwe hatua kama wezi wengine. Mheshimiwa Rais hapendi uonevu, ni mtu wa haki.”
Chanzo; Eatv