Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa fainali za Tuzo za Utalii Duniani zinazotarajiwa kufanyika mwakani (World Travel Awards 2026).
Hayo yameelezwa leo Jumatatu, Desemba 8, 2025 na Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Hassan Abbas baada ya kuwasili nchini kutokea nchini Bahrain ambapo yalifanyika mashindano hayo mwaka huu, huku Tanzania ikishinda tuzo ya kuwa kituo bora cha utalii wa safari duniani.
Amesema Tanzania inapata nafasi ya kuandaa tuzo hizi za dunia baada ya kushinda tuzo hiyo mara mbili mfululizo ikiwa na maana kuwa dunia imeitambua na kuiamini.
“Mwaka jana tuliifuata Ureno mwaka huu tumeifuata Bahrain mwakani dunia inakuja Tanzania haya ni mafanikio ya sisi kuendelea kuhifadhi na kuendeleza utalii, hivyo hatutahangaika kuifuata bali dunia itakuja,” amesema Dk Abbas.
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Ephraim Mafuru amesema dunia imeichagua Tanzania hivyo ni vyema Watanzania kuendelea kuunga mkono sekta ya utalii ili mchango wake ukue kwenye uchumi.
Chanzo; Mwananchi