Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi Aisha Amour, ameielekeza Wakala ya Barabara Tanzania (Tanroads) kufungua kwa muda barabara zote za makutano katika maeneo yanayotekelezwa miradi ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) ili kupunguza msongamano wakati ujenzi ukiendelea.
Balozi Amour ametoa maelekezo hayo leo Jumamosi Desemba 6, 2025 baada ya kukagua maendeleo ya mradi huo jijini Dar es Salaam, akisema hatua hiyo inalenga kupunguza msongamano wa magari kuelekea Sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.
“Tumeona njia ya haraka ya kupunguza msongamano katika kipindi hiki ni kufungua barabara za makutano wakati tukisubiri ujenzi wa kudumu wa barabara hizo unaoendelea, ukiwemo ule wa BRT,”amesema Balozi Aisha.
Mbali na hilo, Balozi Aisha amewaelekeza wakandarasi wote kuhakikisha barabara za michepuko zinapitika na ziko katika hali nzuri.
Pia, amesema mkandarasi anayejenga kipande cha barabara ya Mwenge-Tegeta ameahidi kuweka lami ya muda katika barabara ya mchepuko ili kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji.
“Ili kupunguza malalamiko yanayotokana na msongamano unaosababishwa na utekelezaji wa mradi wa BRT, Tanroads itatoa taarifa za mara kwa mara zitakazowasaidia watumiaji wa barabara kujua njia mbadala ya kutumia wakati wa kwenda na kurudi katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku,” amesema.
Meneja wa Tanroads Mkoa wa Dar es Salaam, Alinanuswe Kyamba amesema wameanza kuyafanyia kazi maelekezo ya Balozi Aisha kwa kuwaelekeza baadhi ya wakandarasi kufungua barabara hizo.
Chanzo; Mwananchi