Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro linafanya uchunguzi wa tukio la waombolezaji wa msiba kuchoma moto magari mawili aina ya Mazda Cx-5 yenye namba za usajili T.214 EJU na Toyota Noah yenye usajili T 350 DCH yaliyotumika kusafirisha mwili wa marehemu kwa ajili ya shughuli za mazishi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa Waandiahi wa Habari na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro SACP Alex Mkama tukio hilo limetokea Disemba 17, 2025 katika Kitongoji cha Kilingeni kijiji cha Lusanga kata ya Diyongoya Tarafa ya Tuariani wilaya ya Mvomero mkoani humo.
Taarifa hiyo imefafanua kuwa, magari hayo yaliyochomwa moto na kuharibika yalitumika kusafirisha mwili wa Mwanahasan Juma Hamis (18) Mfanyakazi wa Nyumbani aliyefariki kwa maradhi Jijini Dar es salaam alipokuwa akifanya kazi yake, kisha kusafirishwa kwao turiani kwa mazishi.
Wakati taratibu za mazishi zikiendelea ndipo ilipotokea taharuki ikihusisha kutilia mashaka ya mazingira ya kifo cha msichana huyo, ndipo wasindikizaji wa marehemu walipofungiwa ndani na wenyeji ili watoe maelezo zaidi kisha magari hayo kuchomwa moto.
Hatahivyo, wasindikizaji hao waliweza kuokolewa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na uongozi wa serikali ya mtaa na sasa linaendelea na uchunguzi na taarifa ya kina itatolewa na jeshi hilo baada ya uchunguzi kukalimika, huku likiendelea pia kuimarisha usalama katika eneo.
Chanzo; Clouds Media