Jeshi la Polisi mkoani Mtwara limemwachia kwa dhamana muuguzi wa Hospitali ya Rufaa ya Ligula, Kulwa Kosmasi, ambaye alikuwa akishikiliwa kwa tuhuma za uchochezi mtandaoni. Kamanda wa Polisi mkoani humo, Issah Suleimani, amethibitisha kuwa muuguzi huyo alihojiwa na kupewa dhamana huku upelelezi wa shauri lake ukiendelea, akisisitiza kuwa mhusika hakutekwa bali alikamatwa kwa kufuata taratibu zote za kisheria za jeshi hilo.
Aidha, Kamanda Suleimani amewasihi wananchi wa Mkoa wa Mtwara kutumia mitandao ya kijamii kwa faida na kuepuka kuitumia kwa nia ovu au kusambaza ujumbe wa uchochezi unaoweza kuhatarisha amani. Hatua hiyo imekuja kufuatia kuenea kwa uvumi kuhusu mazingira ya kukamatwa kwa muuguzi huyo, ambapo Jeshi la Polisi limeweka wazi kuwa litaendelea kusimamia sheria kwa yeyote atakayebainika kukiuka miongozo ya matumizi ya mitandao.
Chanzo; Itv