Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) umetangaza kusimamishwa kwa muda kwa huduma ya Kivuko cha MV KAZI katika eneo la Posta – Kigamboni baada ya kuibuka kwa changamoto kwenye mifumo yake ya uendeshaji.
Kupitia taarifa iliyotolewa leo, Novemba 24, 2025, TEMESA imeeleza kuwa mafundi wake wako katika kivuko hicho wakishughulikia tatizo hilo ili kurejesha huduma haraka iwezekanavyo.
“Mafundi wetu wako kwenye kivuko wakijaribu kutatua changamoto iliyojitokeza. Huduma kwa sasa inaendelea kutolewa na vivuko vya Azam Sea Taxi,” imeeleza taarifa hiyo.
Aidha, TEMESA imewataka watumiaji wa magari, pikipiki na baiskeli kutumia Daraja la Mwalimu Nyerere, kwani vivuko vinavyoendelea kutoa huduma kwa sasa vinabeba abiria pekee.
Wakala huo pia umeomba radhi kwa usumbufu uliojitokeza na kuahidi kutoa taarifa zaidi pindi matengenezo yatakapokamilika.
Chanzo; Nipashe