Mtoto wa miaka mitano, David Chuwa, mkazi wa Mtaa wa Kariwa Chini, Kata ya Rau, Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, amegundua kifo cha bibi yake, Mchungaji wa Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT) Makimbilio, Jane Mwangalimi, aliyefariki dunia nyumbani walikokuwa wakiishi pamoja.
Taarifa zinaeleza kuwa tukio hilo lilitokea Januari 20, 2026, baada ya mtoto huyo kuamka asubuhi na kumuita bibi yake mara kadhaa ili amuandalie chakula, bila kupata majibu yoyote.
Akisimulia tukio hilo, mtoto huyo amesema baada ya kumuita kwa muda mrefu bila mafanikio, alijaribu kumgusa bibi yake na kubaini kuwa alikuwa anatokwa na damu mdomoni.
“Niliendelea kumuita bibi bila mafanikio, nikaenda kucheza, lakini njaa iliendelea kuniuma. Nikarudi tena kwa bibi na kuona anatokwa damu mdomoni. Nikaenda mlangoni, nikaweka kiti nikaufungua ili niende kwa mama lovu kula chakula. Nilimueleza tukarudi pamoja kumtazama bibi,” amesema mtoto huyo.
Akizungumza kuhusu tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, amesema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya KCMC kwa ajili ya uchunguzi wa kitabibu ili kubaini chanzo cha kifo.
Amesema uchunguzi huo ni muhimu siyo tu kubaini chanzo cha kifo, bali pia kuondoa hofu kwa jamii.
Mmoja wa majirani wa marehemu, Calista Lyimo, amesema usiku wa kuamkia siku ya tukio walikuwa pamoja katika ibada ya maombi ya jioni, ambapo marehemu alilalamika kujisikia vibaya kidogo, jambo ambalo halikuwatia shaka kubwa.
Amesema hakutegemea kuwa hiyo ingekuwa mara ya mwisho kumuona marehemu akiwa hai.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Kariwa Chini, Thomas Materu, amesema baada ya kupokea taarifa kutoka kwa balozi wa mtaa, alifika eneo la tukio na kuthibitisha kifo hicho kabla ya kuwataarifu vyombo vya ulinzi na usalama kwa hatua zaidi.
Chanzo; Nipashe