Wananchi wa maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam na Pwani wamedai kukabiliwa na adha kubwa ya upatikanaji wa maji, wakikosa huduma kwa zaidi ya wiki mbili.
Hali hiyo imewalazimu wakazi wengi kutumia muda mwingi kutafuta maji, huku gharama zikipanda maradufu na kuongeza mzigo katika maisha yao ya kila siku, wengine wakihofu kupata magonjwa ya mlipuko.
Katika maeneo ya Kibaha (Pwani) na Msasani, Kinondoni na baadhi ya maeneo ya Tabata na Goba jijini Dar es Salaam, wakazi wanasema maji yamekuwa yakitoka kwa nadra au kutotoka kabisa, hali inayowalazimu kununua maji ya madumu kwa bei kubwa ambayo imepanda ghafla kutokana na uhaba uliopo.
“Wiki ya pili sasa hatujapata maji, tuliambiwa huwa yanatoka saa 8 usiku, tumeamka wiki nzima muda huo ili kuona kama tutapata maji lakini napo hayatoki," amesema Odiria Lutumo wa Kibaha kwa Mfipa.
Mkazi wa Kinondoni Biafra, Neema Mussa amesema kila wanapofikiria watapata wapi maji ya kupikia na kuoga, wanakata tamaa na kuichukia nyumba yao.
“Tunapika kwa kupima maji, kuoga imefikia hatua tunaona si lazima tena, kwangu tulikuwa tunaoga asubuhi na jioni lakini sasa ni mara moja tena kwa maji kidogo sana ili kupunguza matumizi, achilia mbali hata kufua tumeshindwa, maisha bila maji yamekuwa ya mateso,” amesema.
Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasa), Everlasting Lyaro alipoulizwa na Mwananchi juu ya uhaba huo wa maji katika baadhi ya maeneo ya Pwani na Dar es Salaam amesema, kwenye uzalishaji hakuna changamoto ya maji.
"Mpaka sasa hatuna changamoto kwenye uzalishaji wa maji, kwa siku na hata inapotokea tumepata hitilafu katika mitambo na kunahitajika matengenezo tunatoa taarifa mapema," amesema.
Chanzo; Mwananchi