Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Said Kabuga amefariki dunia baada ya kutumbukia kwenye kisima huku taarifa zikieleza kuwa ni hofu ya kupoteza fedha nyingi kwenye kamali.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gallus Hyera amethibitisha tukio hilo akisema taarifa za awali zinaonyesha alijitupa mwenyewe kisimani.
Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo Jumatano Novemba 26, 2025 ambapo simu na vifaa vingine vimekutwa juu ya kisima hicho.
"Ni kweli taarifa hizo tunazo, lakini kinachoonyesha ni kwamba alijitupa kisimani mwenyewe kwa kujiandaa na bado kuna mambo tunayachunguza," amesema Kamanda Hyera.
Kwa mujibu wa wanafunzi wenzake, Kabuga alikuwa mwaka wa pili anasoma Shahada ya Uandishi wa Habari na Uhusiano wa Umma na inaelezwa hakuwa na tatizo katika maisha yote akiwa mwaka wa kwanza chuoni hapo.
"Naomba msiniandike jina langu, lakini jamaa alibeti jana fedha za ada na baadaye alianza kulalamika kuwa itakuwaje kwa wazazi wake, ile hofu hata chakula cha jioni hakula," amesema mmoja wa wanafunzi.
Chanzo; Mwananchi