Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa watatu kwa tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi zenye uzito wa kilo 168, pamoja na watuhumiwa wengine watatu kwa tuhuma za wizi wa pikipiki.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, watuhumiwa wa kesi ya dawa za kulevya ni Mseveni Menat, mkazi wa Uyole; Fred Lulandala, mkazi wa Mapelele; na Joseph Ngelenge, mkazi wa Uyole jijini Mbeya.
Watuhumiwa hao walikamatwa Januari 21, 2026 katika Stendi Kuu ya Mabasi jijini Mbeya, wakiwa kwenye Bajaj yenye namba za usajili MC 850 EWN aina ya TVS King’s.
Ilielezwa kuwa dawa hizo za kulevya zilikuwa zimefungwa kwenye mabegi manane, na watuhumiwa walikuwa wakizisafirisha kuelekea jijini Arusha.
Uchunguzi wa awali unaonesha kuwa bangi hiyo iliingizwa nchini kutoka nchi jirani na ilipangwa kusafirishwa kwa njia ya basi.
Jeshi la Polisi limeeleza kuwa uchunguzi unaendelea ili hatua zaidi za kisheria zichukuliwe dhidi ya wahusika.
Chanzo; Global Publishers