Hali ya usafiri katika eneo la Shekilango jijini Dar es Salaam imekuwa changamoto huku idadi ya abiria wanaosaka safari za kwenda mikoani ikiongezeka mapema kuliko ilivyozoeleka miaka ya nyuma.
Kwa kawaida, misururu ya abiria huanzia Desemba 20 kuelekea Sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.
Hata hivyo, safari hii msongamano huo umejitokeza mapema, jambo lililowashangaza hata wasafirishaji wa magari ya mikoani.
Katika eneo hilo maarufu kwa vituo vidogo vya mabasi na ofisi za makampuni ya usafirishaji, hali ya hekaheka imetawala, kuanzia asubuhi ya leo Jumatano, Desemba 3, 2025 huku foleni za abiria na magari zikisababisha usumbufu na kukwamisha huduma za usafiri.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na Mwananchi wamekiri awali walipanga kusafiri baadaye, lakini wameamua kuondoka mapema kufuatia tetesi za mitandaoni kuhusu yanayohofiwa yanaweza kutokea Desemba 9.
Hivyo wamesema hawataki kuhatarisha safari zao au kuhofia kukosa usafiri endapo hali ya usalama itabadilika. Wengine wamedai taarifa zinazosambaa mtandaoni zimeongeza presha na kuwalazimu kutafuta usafiri mapema.
Hadi saa 5 asubuhi, uwingi wa abiria Shekilango umeongeza shinikizo kwa watoa huduma za usafirishaji, huku wamiliki wa magari wakilazimika kuongeza safari ili kukidhi mahitaji jambo wanalofurahia kwa kuwa wanaongeza kipato
Chanzo; Mwananchi