Mfanyabiashara wa Tanzania, Mohammed Dewji maarufu kama Mo, ameendelea kushika nafasi ya kwanza kwa utajiri katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati akiwa na utajiri unaokadiriwa kufikia takribani Sh trilioni 5.45 za Kitanzania.
Kwa mujibu wa ripoti mpya ya jarida la Forbes iliyotolewa Machi 9, Dewji anaongoza orodha ya matajiri katika ukanda huo huku akishika nafasi ya 14 katika bara la Afrika.
Katika orodha hiyo, bilionea kutoka Nigeria, Aliko Dangote ameendelea kuongoza kama mtu tajiri zaidi barani Afrika.
Dewji ni Mkurugenzi Mtendaji wa MeTL Group, kampuni kubwa ya biashara inayojishughulisha na uzalishaji na usambazaji wa bidhaa mbalimbali za vyakula ikiwemo unga wa ngano, mafuta ya kula, usagaji wa nafaka pamoja na uzalishaji wa vinywaji.
Kampuni hiyo ilianzishwa na baba yake katika miaka ya 1970 na baadaye kuendelezwa kwa mafanikio na Dewji, ambaye ameipanua biashara hiyo hadi kuvuka mipaka ya Tanzania. Kwa sasa, MeTL Group inaendesha shughuli zake katika zaidi ya nchi 10 barani Afrika, zikiwemo Uganda, Ethiopia na Kenya.
Mbali na shughuli zake za biashara, Dewji mwenye umri wa miaka 50 pia ni mwekezaji na Rais wa klabu kongwe ya soka nchini, Simba SC.
Ripoti ya Forbes pia imebainisha kuwa utajiri wa mabilionea barani Afrika unaendelea kuongezeka kwa kasi. Kwa sasa, matajiri wakubwa 23 wa bara hilo wanakadiriwa kuwa na utajiri wa pamoja unaofikia dola bilioni 126.7 za Marekani.
Kwa upande wake, Dangote anaendelea kushika nafasi ya kwanza akiwa na utajiri unaokadiriwa kufikia dola bilioni 28.5. Utajiri wake umeongezeka kwa dola bilioni 4.6 mwaka huu kufuatia kupanda kwa karibu asilimia 69 ya hisa za kampuni yake ya saruji, Dangote Cement, ambayo pia iliongeza faida zake maradufu mwaka 2025 hadi kufikia rekodi ya naira trilioni moja.
Mfanyabiashara mwingine aliyepata ongezeko kubwa zaidi la utajiri ni Abdulsamad Rabiu, ambaye utajiri wake umeongezeka kwa asilimia 120 na kufikia dola bilioni 11.2, na hivyo kuwa mtu wa tatu tajiri zaidi barani Afrika.
Chanzo; Clouds Media