Ikiwa tunaeleka ukingoni mwa mwaka 2025, leo zimetimia siku 222 tangu kutekwa kwa kada wa Chama cha Demokrasia na Maendelo (CHADEMA) Mdude Nyagali na watu wasiojulikana usiku wa Mei 2 mwaka huu akiwa nyumbani kwake mkoani Mbeya.
Kwa mujibu wa mkewe, Sije Mbugi aliyesimulia tukio hilo na kunukuliwa na vyombo vya habari, anasema wakiwa nyumbani kwao Mtaa wa Iwambi, Jijini Mbeya walisikia sauti za watu wakijaribu kufungua geti, yeye akiwa wa kwanza kusikia alimuamsha na mumewe baada ya muda mfupi walifanikiwa kuvunja geti kisha mlango wa chumba walicholala na kuingia ndani.
Yeye na mumewe anaeleza walijitahidi kupambana lakini walizidiwa nguvu na watu hao ambao walifanikiwa kumchukua Mdude na kuondoka nae kusikojulikana na hadi leo haijulikani alipo.Hali ikiwa hivyo kwa Mdude Nyagali, aliyewahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole yeye inadaiwa alivamiwa na watu wasiojulikana usiku wa Oktoba 6 mwaka huu.

Picha zilizosambaa mitandaoni zilionesha nyumba yake ikiwa imevunjwa milango huku michirizi ya damu ikionekana sakafuni kuonesha huenda palikuwapo na mapambano ya kujitetea dhidi ya watekaji na hivyo huenda alijeruhiwa na watu hao wakati wa mapambano baina yao.
Tangu wakati huo zimetimia siku 65 bila Polepole kuonekana hadharani huku Jeshi la Polisi nchini likiahidi kuendelea kufuatilia matukio hayo na mengine ya aina hiyo kwa karibu ili kuyadhibiti.
Chanzo; Nipashe