Kipa wa Azam FC, Aishi Manula, ameitwa katika kikosi cha Timu ya Taifa (Taifa Stars), kitakachoingia kambini kujiandaa na michezo miwili ya kirafiki ya kimataifa (FIFA Series 2026), itakayofanyika Kigali, Rwanda hivi karibuni.
Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Miguel Gamondi, amesema amemwita Manula kutokana na ubora na uzoefu aliokuwa nao kipa huyo wa zamani wa Simba.
"Manula ni kati ya makipa wazuri na wa muda mrefu, hivyo ninaamini kuelekea kwenye FIFA Series ataipa mafanikio timu ya Taifa," amesema Gamondi.
Kocha huyo amesema ameamua kujumuisha wachezaji chipukizi kutokana na kuridhishwa na uwezo wao na hajaita mchezaji kwa ukubwa wa timu anayochezea isipokuwa viwango walivyonavyo.
“Malengo ni kuona Timu ya Tanzania inafanya vizuri katika mashindano mbalimbali, naomba mashabiki waendelee kuiunga mkono timu hii ili iweze kufanikisha malengo yake,” Gamondi amesema.
Mbali na Manula, nyota wengine walioitwa ni pamoja na Idd Suleiman, Zuberi Foba, Elias Lameck, Feisal Salum kutoka Azam FC, Nickson Kibabage, Yusuph Kagoma, Selemani Mwalimu (Simba), Bakari Mwamnyeto, Mudathir Yahya, Ibrahim Abdullah (Yanga) , Mohamed Mussa (Mashujaa FC), Yona Amosi , Kelvin Nashon, (Pamba Jiji), Haji Mnoga (Salford City), Saimon Msuva (Al Talabaq), Charles M’mombwa (Florida FC Malta), Tarryn Allarakhia (Rochdale FC) na Paul Peter wa JKT Tanzania.
Katika michezo hiyo ya FIFA Series, Taifa Stars imepangwa Kundi B pamoja na Aruba, Macau na Liechtensten.
Chanzo; Nipashe