Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro, amesema idadi ya wahamiaji wanaokimbia machafuko katika mji wa Uvira, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), imeongezeka na kufikia watu 202.
Kauli hiyo inakuja siku moja baada ya ripoti kuonesha waasi wa M23, waliokuwa wakipambana na Jeshi la DRC, wameachia mji wa Uvira.
Hata hivyo, idadi ya raia wanaovuka mpaka na kuingia Tanzania kutafuta hifadhi na usalama imeendelea kuongezeka.
Kwa mujibu wa Balozi Sirro, Desemba 14, 2025, walikamatwa wahamiaji 52, huku jana, Jumanne, Desemba 16, 2025, wakikamatwa wengine 150. Wote walikamatwa wakiwa kwenye vyombo vya usafiri na wakiwa wamechanganyika na raia wa kawaida wa Tanzania.
Akizungumza na Mwananchi leo, Desemba 17, 2025, Balozi Sirro, ambaye pia ni Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) mstaafu, amesema kukamatwa kwa wahamiaji hao ni sehemu ya operesheni zinazoendelea za kulinda ulinzi na usalama mkoani Kigoma.
“Jana tumewakamata wahamiaji wengine 150, na hivyo jumla yao kufikia 202. Wote wanaendelea kuhojiwa na vyombo vya ulinzi na usalama, na taratibu zikikamilika tutawakabidhi UNHCR kwa ajili ya kupelekwa makambini,” amesema.
Chanzo; Mwananchi