Mahakama Kuu ya Tanzania Masijala Ndogo ya Dar es Salaam imetupilia mbali kesi ya kudharau amri ya mahakama iliyokuwa inawakabili Viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Kesi hiyo yenye maombi 24850 ya mwaka 2025 ilifunguliwa na Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Zanzibar Saidi Issa Mohamed na wenzake akiiomba mahakama itoe amri ya kuwakamata na kuwaweka Gerezani Viongozi waandamizi wa CHADEMA akiwemo Makamu Mwenyekiti, John Heche.
Uamuzi huo umetolewa leo na Jaji Awamu Mbagwa aliyesema anakubaliana na mapingamizi ya Wakili wa utetezi, Hekima Mwasipu kuwa maombi hayo yameletwa Mahakamani hapo nje ya muda.
“Leo ilipangwa itolewe uamuzi kama mapingamizi yana msingi ama lah, Jaji amesoma uamuzi ikiwemo hoja ya ukomo wa madai(ndani ya muda) kwamba yaletwe ndani ya siku 60 tangu malalamiko yatokee, zimeshapita hizo siku na Jaji ametupilia mbali bila gharama,” amesema Mwasipu nje ya mahakama.
Chanzo; Millard Ayo