Serikali imetangaza rasmi kuanza utekelezaji wa Bima ya Afya kwa wote awamu ya kwanza kwa kundi la wananchi wasio na uwezo (wazee, watoto, wajawazito na walemavu) ambao watagharamiwa na Serikali pamoja na kutangaza kitita cha huduma muhimu kitakachotolewa na skimu za Bima ya Afya kwa gharama ya Shilingi 150,000 kwa Kaya ya watu wasiozidi 6.
Hayo yamesemwa Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa leo Januari 23, 2026 Jijini Dodoma kwenye kikao cha kujadili utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote na Viongozi na Watendaji ngazi ya Mikoa, Wilaya pamoja na Serikali za Mitaa.
Wazir Mchengerwa ametangaza kuanza rasmi kwa Bima ya Afya kwa wote Januari 26, 2026 na kuwataka watendaji kuhakikisha wananchi wanapata elimu kabla ya kujiunga na huduma bora za afya kuendelea kutolewa kwa wananchi wakiwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kote nchini.
Waziri Mchengerwa amesema kuwa kwa gharama ya Shilingi 150,000 watu 6 walio kwenye kaya moja watajiunga na Bima ya Afya kwa wote kwa itakayojumuisha mwanachama mchangiaji, mwenza wa mwanachama na wategemezi wanne (4).
“Wategemezi hao wanne wanaweza kuwa ni mzazi wa mwanachama au mzazi wa mwenza wa mwanachama; mtoto wa mwanachama wa kuzaa, kuasili au wa kambo aliye na umri chini ya miaka ishirini na moja au ndugu wa damu wa mwanachama aliye na umri wa chini ya miaka ishirini na moja” amefafanua Waziri Mchengerwa.
Amesema kuwa kitita cha Huduma Muhimu kitatolewa kwa kuzingatia utaratibu wa rufaa katika vituo vya kutolea huduma za Afya vitakavyoingia Mkataba na skimu za Bima ya Afya.
Waziri Mchengerwa amesema ili kufikia azma ya uhakika wa matibabu kwa wananchi wote kupitia Bima ya Afya Viongozi na Watendaji hawana budi kuhakikisha kuwa elimu sahihi inawafikia wananchi waweze kujua umuhimu wa kuwa na Bima ya Afya.
Chanzo; Bongo 5