Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani Kilimanjaro limemkamata na kumwadhibu dereva wa gari ya Shule moja ya Msingi Wilaya ya Moshi, akituhumiwa kuendesha akiwa katika hali ya ulevi, huku akiwa amebeba wanafunzi zaidi ya kumi, jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa wanafunzi hao.
Akizungumzia tukio hilo leo Jumatano, Machi 18, 2026, kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani mkoa wa Kilimanjaro, ACP Nassor Sisiwaya, dereva huyo amekamatwa Barabara Kuu ya Moshi-Arusha, Manispaa ya Moshi wakati wa operesheni maalumu ya ukaguzi wa magari na upimaji wa ulevi kwa madereva, inayoendelea mkoani humo kwa lengo la kudhibiti ajali za barabarani.
Kutokana na hali hiyo dereva huyo, Emmanuel Kawiche amefungiwa leseni miezi sita, huku wamiliki wa shule wakishauriwa kununua vifaa vya kupimia ulevi, ili kuweza kuwapima madereva wa magari ya shule kabla ya kuwakabidhi magari.
Amesema Jeshi la Polisi limejipanga kuhakikisha madereva wote wanazingatia sheria za usalama barabarani, hususani wanaosafirisha wanafunzi na kusisitiza kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atakayekiuka sheria hizo ili kulinda maisha ya watumiaji wa barabara.
Chanzo; Mwananchi