Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limeendelea kutoa mafunzo kwa vijana wa Kitanzania kupitia mifumo miwili, ambayo ni mafunzo ya kujitolea na mafunzo ya kwa mujibu wa sheria.
Kwa sasa, JKT limetangaza nafasi za kujiunga na mafunzo ya kujitolea, ambapo kipaumbele kimetolewa kwa vijana waliobobea katika masomo ya sayansi ya teknolojia na usalama wa mtandao (Cyber Security).
Akizungumza katika Makao Makuu ya JKT jijini Dodoma, Mkuu wa Tawi la JKT Makao Makuu, Brigedia Hassan Mabena, amesema kuwa usaili wa waombaji utaanza rasmi Januari 26, 2026.
Amesisitiza kuwa mchakato wa kujiunga na JKT ni bure kabisa, na unaanzia ngazi ya wilaya ili kutoa fursa sawa kwa vijana wote wenye sifa.
Brigedia Mabena ameongeza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikiendesha mafunzo hayo kupitia JKT kwa lengo la kuimarisha uzalendo, nidhamu na stadi za maisha kwa vijana.
Amesema vijana wanaojiunga hupata mafunzo kwa kipindi cha miaka mitatu, yakijumuisha mafunzo ya kijeshi, maadili ya kazi pamoja na ujuzi mbalimbali unaowawezesha kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.
Chanzo; Global Publishers