Morogoro. Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro limewakamata watu sita kwa tuhuma za mauaji ya mkulima mkaazi wa Bwala la Kihonda, Sweeya John Sweeya (70) aliyefariki dunia baada ya kushambuliwa na kundi la watu waliodaiwa kujichukulia sheria mkononi, huku majina ya watuhumiwa hao yakihifadhiwa kwa sababu za kiuchunguzi zaidi.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Kamishna msaidizi mwandamizi wa Polisi Alex Mkama, tukio hilo limetokea Januari 22, 2026 majira ya saa 11 alfajiri ambapo mwili wa marehemu ulikutwa kwenye kichaka karibu na Bwala la Kihonda, lililopo katika Kitongoji cha Sokoine Ranchi, Kijiji cha Wami Sokoine, Kata ya Dakawa, Wilaya ya Mvomero.
Kamanda Mkama ameeleza kuwa marehemu Sweeya, alishambuliwa kwa kupigwa na vitu butu kichwani na kikundi cha watu waliodaiwa kujichukulia sheria mkononi hali iliyosababisha kupoteza maisha yake kabla ya kupatiwa msaada wa kitabibu.
Upelelezi wa awali wa Jeshi la Polisi umebaini kuwa chanzo cha tukio hilo ni mgogoro wa ardhi baina ya kikundi cha watu waliovamia na kuweka makazi katika eneo la Ranchi ya Dakawa na wamiliki halali wa ardhi hiyo.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro limetoa wito kwa wananchi kutumia mkondo wa sheria katika kutafuta suluhu ya migogoro inayohusu ardhi na kuacha vitendo vya kujichukulia sheria mkononi, likisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wote watakaobainika kuhusika na tukio hilo.
Chanzo; Mwananchi