Kiangazi cha muda mrefu pamoja na kuongezeka kwa shughuli za kibinadamu katika maeneo ya vyanzo vya maji kimeelezwa kuathiri upatikanaji wa maji katika Mkoa wa Morogoro.
Akizungumza na watendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (MORUWASA), Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, amesema uzalishaji wa maji katika vyanzo vinavyotegemewa na wakazi wa mkoa huo umepungua kwa asilimia 75. Kwa sasa, maji yanayopatikana ni asilimia 25 ya kiwango cha kawaida.
Pia ameiagiza MORUWASA kupanga ratiba za mgao zinazoeleweka na kuzifuatilia kwa karibu, huku akisisitiza umuhimu wa kulinda vyanzo vya maji ili kuepusha athari za uharibifu wa mazingira na uchepushaji maji
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa MORUWASA, CPA Sais Kyejo, amesema kupungua kwa maji kumesababisha mamlaka kutoa huduma kwa mgao. Ameeleza kuwa kawaida MORUWASA huzalisha lita za ujazo milioni 20 kwa siku, lakini kutokana na hali ya sasa, uzalishaji umeshuka hadi lita za ujazo milioni 5 kwa siku.
Chanzo; Crown Media