Mahakama Kuu ya Uhujumu Uchumi, Divisheni ya Makosa ya Rushwa, imemhukumu kifungo cha miaka 28 jela mshtakiwa David Kanayo Chukwu, raia wa Nigeria, baada ya kukiri kosa la kushiriki katika kusafirisha kilogramu 268.50 za dawa za kulevya aina ya heroin.
Hukumu hiyo ilisomwa Januari 22, 2026, na Hakimu Otaru Joachimu, ambaye alisema mahakama imezingatia kipindi cha miaka mitano na miezi tisa ambacho mshtakiwa huyo amekaa mahabusu tangu alipokamatwa. Kutokana na hilo, atatumikia kifungo cha miaka 22 na miezi mitatu iliyobaki ili kukamilisha adhabu hiyo.
Katika hatua nyingine, mahakama hiyo imemuondolea mashtaka mshtakiwa wa tatu, Alistair Amon Mbele, baada ya Jamhuri kushindwa kuthibitisha kosa dhidi yake katika shauri namba DCEA/IR/06/2020 ECO 36/2020. Shauri hilo linawahusisha David Kanayo Chukwu (raia wa Nigeria), Isso Lomward Lupembe (raia wa Tanzania) na Alistair Amon Mbele (raia wa Tanzania).
Kwa upande wa mshtakiwa wa pili, Isso Lomward Lupembe, kesi yake inaendelea katika mahakama hiyo baada ya kukana shtaka linalomkabili.
Aidha, mahakama imeagiza kuwa shauri la jarada la mali za watuhumiwa hao (asset forfeiture) linapaswa kushughulikiwa ndani ya kipindi cha mwaka mmoja kuanzia tarehe ya kusomwa kwa hukumu hiyo.
Watuhumiwa hao walikamatwa mwaka 2020 na maafisa wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) katika eneo la Mbezi Kibanda cha Mkaa, jijini Dar es Salaam, wakituhumiwa kusafirisha kilogramu 268.50 za dawa za kulevya aina ya heroin.
Shauri hilo limeahirishwa hadi Februari 23, 2026, kwa hatua zaidi za kisheria.
Chanzo; Nipashe