Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimefungua kesi katika Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ) ikikilalamikia hatua ya Serikali ya kuzima mtandao kuanzia Oktoba 29 hadi Novemba 4, 2025.
Kesi hiyo namba 56/2025 imewasilishwa Desemba 3,2025 ikiomba mahakama itamke kuwa kuzimwa kwa huduma za intaneti ilikiuka vifungu 6(d), 7(2) na 8(1)(c) vya Mkataba wa EAC wa mwaka 1999.
Mbali na kutamka hivyo, pia LHRC inaiomba mahakama ya EACJ kutoa amri inayozuia Serikali kurudia tena kuzima mtandao bila sheria au amri halali ya mahakama.
Kesi hiyo inayowakilishwa na mawakili wa LHRC, Wakili Peter Majanjara na Wakili Jebra Kambole.
Majanjara amesema kuwa wamefikia hatua ya kufungua kesi hiyo kutokana na kuzimwa kwa mtandao ghafla saa tano asubuhi siku ya Oktoba 29 na kuathiri huduma zote za mawasiliano nchini kwa siku saba mfululizo.
Chanzo; Mwananchi