Wananchi wa Kitongoji cha Mtakuja Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro wamepata furaha baada ya Mnyama Kakakuona kuonekana katika eneo lao na kuchagua mazao mbalimbali badala ya Silaha.
Baadhi ya wananchi waliofika katika eneo hilo wamesema licha ya kuwekewa mazao mbalimbali, silaha ,maji lakini mnyama huyo amechagua zao la Mahindi,Mpunga na Alizeti huku akishindwa kuchagua Silaha na maji jambo ambalo wameona ni neema kwani angechagua Silaha kungekuwa na Machafuko huku angechagua maji kungekuwa na Mafuriko.
Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Maulid Dotto amewashukuru wananchi kwa kutimiza wajibu wao na kutoa taarifa kwa wakati, akisema kitendo hicho kinaonesha uelewa mzuri wa jamii kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa wanyamapori.
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya amesema kuwa mnyama huyo pindi anapoonekana huonyesha ishara mbalimbali kulingana na mila na desturi za jamii, huku akibainisha kuwa Kakakuona huyo ameonesha ishara ya uwepo wa mavuno mengi hususan katika mazao ya mahindi na mpunga baada ya kumuwekea mbegu za mazao hayo, hivyo hakutakuwa na Changamoto ya chakula.
Afisa Wanyamapori wilaya hiyo Bi. Avelin Maingu amebainisha kuwa katika Wilaya hiyo kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita Kakakuona ameonekana zaidi ya mara tano na kuongeza kuwa hiyo ni ishara ya neema katika Wilaya hiyo.
Chanzo; Millard Ayo