Nchi za Ujerumani na Austria zimetangaza kuanza kuachia sehemu ya akiba yao ya mafuta kufuatia ombi la Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IEA) kwa nchi wanachama kutoa jumla ya mapipa milioni 400 ya mafuta, ili kupunguza kupanda kwa bei ya nishati duniani kunakosababishwa na vita vya Iran.
Hatua hiyo inakuja wakati hali ya soko la nishati duniani ikiendelea kuwa tete kutokana na mvutano wa kijeshi Mashariki ya Kati. Pia Japan imetangaza itaanza kuachia sehemu ya akiba yake ya mafuta kuanzia Jumatatu ijayo.
Kwa mujibu wa ABC News mawaziri wa nishati wa nchi za Group of Seven (G7) walikutana Jumanne makao makuu ya IEA mjini Paris, Ufaransa, kujadili hatua za kukabiliana na kupanda kwa bei ya nishati hiyo muhimu.
Mkurugenzi Mkuu wa IEA, Fatih Birol amesema wamejadili mbinu zote ikiwa ni pamoja na kutoa hifadhi ya dharura ya mafuta ya shirika la IEA na kuruhusu kuingia kwenye soko la dunia.
Kwa mujibu wa IEA, hatua kubwa zaidi kuwahi kuchukuliwa hapo awali ya kuachia akiba za dharura ilikuwa mapipa milioni 182.7 mwaka 2022 kufuatia upungufu wa nishati uliosababishwa na uvamizi kamili wa Russia nchini Ukraine.
Kwa sasa, nchi wanachama wa IEA zinamiliki zaidi ya mapipa bilioni 1.2 ya akiba ya mafuta ya dharura inayomilikiwa na serikali, huku sekta binafsi ikiwa na takriban mapipa milioni 600 chini ya usimamizi wa serikali.
Chanzo; Mwananchi