Imefahamika kwamba wanamgambo wa RSF nchini Sudan walifaya mauaji ya watu wengi katika jimbo la Darfur na kisha kujaribu kuficha ushahidi kwa kuwazika kwenye makaburi ya pamoja.
Naibu Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC, Nazhat Shameem Khan, ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba ofisi yake inaamini kuwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinaadamu ulitendeka wakati RSF ilipotwaa udhibiti wa mji mkuu wa Darfur, El-Fasher, mwezi Oktoba.
Kupitia hotuba yake ya jana kwa njia ya video, Khan alisema wana ushahidi wa sauti na picha za video, na za satalaiti kuthibitisha tuhuma zao.
Tangu Aprili 2023, vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya jeshi rasmi la serikali na waasi hao wa RSF vimeshauwa maelfu ya raia na kuwasababisha wengine milioni 11 kuwa wakimbizi, katika kile Umoja wa Mataifa unachosema ni mzozo mkubwa zaidi wa wakimbizi na njaa duniani kwa sasa.
Kumekuwa na ripoti za mauaji ya halaiki, ubakaji, utekaji na wizi tangu RSF kuutwaa mji wa El-Fasher, iliyokuwa ngome ya mwisho ya jeshi la serikali jimboni Darfur. Pande zote mbili zinashutumiwa kutenda ukatili kwenye vita hivyo.
Chanzo; Dw