Mfalme Mswati, mtawala wa kifalme mwenye mamlaka kamili, anadaiwa kumpa aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Joseph Kabila, uraia wa Eswatini bila kufuata sheria ya uraia, kulingana na uchunguzi huru uliofanywa na gazeti la Swaziland News.
Kupewa uraia wa Kabila kunakuja ikiwa ni miezi michache imepita baada kuhukumiwa adhabu ya kifo na Mahakama ya Kijeshi ya DRC kwa tuhuma za kuwa na uhusiano na waasi wa M23, na alipatikana na hatia ya uhaini, uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu.
Swaziland News kwenye ripoti yake imedai kuwa ushahidi wa nyaraka uliopatikana kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Eswatini unaonyesha kuwa, kufuatia agizo la Mfalme kuelekeza Bodi ya Uraia kumpa aliyekuwa Rais wa DRC uraia, Wizara ya Mambo ya Ndani iliendelea kumpa pasipoti ya kidiplomasia.
Taarifa ya gazeti hilo imeendelea kudai kuwa Jumamosi ya Novemba 29, 2025, Kabila aliondoka Eswatini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa King Mswati akitumia pasipoti yake mpya ya kidiplomasia ya Eswatini.
Kwa mujibu wa gazeti hilo mfumo wa Uhamiaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani unaonyesha kuwa hiyo ilikuwa safari yake ya kwanza kutumia pasipoti ya Eswatini.
Gazeti hilo limedai kuwa pasipoti mpya ya kidiplomasia aliyopatiwa Kabila, ikiwemo namba ya pasipoti, haiwezi kuwekwa wazi kwa sababu za kimaadili, kwani kufanya hivyo kunaweza kuhatarisha usalama wake.
Chanzo; Mwananchi