Kiongozi wa upinzani nchini Uganda, Bobi Wine, amesema hatapinga matokeo ya uchaguzi uliofanyika Alhamisi kupitia mahakama, akieleza kukosa imani na mhimili wa haki nchini humo.
Badala yake, amewahimiza wafuasi wake kutumia njia za amani, ikiwemo maandamano ya kisheria, kulinda demokrasia yao.
Akizungumza na BBC akiwa mafichoni, Bobi Wine alisema ataendelea kumpinga Rais Yoweri Museveni licha ya hofu inayohusiana na usalama wake binafsi.
“Mahakama nchini Uganda imepoteza uhuru wake, na tunawahimiza raia kutumia njia zote halali kupinga udhalimu na kulinda demokrasia,” alisema mwanamuziki huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 43.
Rais Yoweri Museveni, mwenye umri wa miaka 81, alitangazwa mshindi wa uchaguzi huo kwa ushindi mkubwa.
Ameishutumu kambi ya upinzani kwa kujaribu kubatilisha matokeo kwa kutumia vurugu, na kuwaita “magaidi”.
Katika mahojiano hayo, Bobi Wine pia alikosoa vikali vyombo vya usalama kwa kuzuia uingizaji wa chakula katika makazi ya familia yake, ambako mke wake na jamaa zake wanadaiwa kuwekwa chini ya kifungo cha nyumbani kwa vitendo.
Alisema alilazimika kuondoka katika nyumba hiyo, iliyoko katika kitongoji cha mji mkuu Kampala, usiku wa Ijumaa kufuatia uvamizi wa vikosi vya usalama.
Chanzo; Bongo 5