Urusi imesema hakuna muafaka kuhusu Ukraine baada ya mazungumzo ya saa tano kati ya Putin na wajumbe wa Trump katika Ikulu ya Kremlin. Hatua hiyo imezua wasiwasi Ulaya na Kyiv, huku pande zote zikisisitiza haja ya mazungumzo zaidi.
Urusi imetangaza kuwa mazungumzo ya saa tano kati ya Rais Vladimir Putin na wajumbe wa Rais Donald Trump katika ikulu ya Kremlin hayakuzaa makubaliano kuhusu mpango wa amani wa kumaliza vita vya Ukraine, ikiwa ni ishara kuwa safari ya kidiplomasia bado ni ndefu.
Trump, ambaye mara kwa mara ameeleza kukerwa na kushindwa kwa Marekani kumaliza mgogoro huo wa Ulaya, alituma mjumbe wake maalumu Steve Witkoff na mkwewe Jared Kushner kuongoza mazungumzo hayo yaliyodumu hadi usiku wa manane.
Mshauri wa ngazi ya juu wa Kremlin kuhusu masuala ya nje, Yuri Ushakov, alisema baadhi ya mapendekezo ya Marekani hayakukubalika kwa Moscow, huku akiongeza kuwa bado kuna kazi kubwa mbele ya pande zote.
Chanzo; Dw