Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, amewataka washirika wa Ulaya kuionyesha Urusi kuwa vita inavyoendesha dhidi ya Kyiv havina maana wala mafanikio.
Zelensky ametoa wito huo kabla ya mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya unaotarajiwa kufanyika Alhamisi mjini Brussels, akisisitiza kuwa maamuzi yatakayofikiwa katika mkutano huo yanapaswa kuifanya Urusi itambue kuwa kuendelea na vita hadi mwaka ujao hakutakuwa na manufaa yoyote.
Amesema Ukraine itaendelea kupata uungwaji mkono wa washirika wake wa kimataifa, jambo litakalodhoofisha dhamira ya Urusi ya kuendeleza vita hivyo.
Wakati huo huo, Kansela wa Ujerumani, Friedrich Merz, ameitaka Umoja wa Ulaya kutumia mali za Urusi zilizozuiliwa kusaidia Ukraine, hatua ambayo amesema itaongeza shinikizo kwa Rais wa Urusi, Vladimir Putin, na kutuma ujumbe wa wazi kwamba Ulaya iko imara katika kuunga mkono Ukraine.
Kauli hizo zinaendelea kuashiria msimamo wa Umoja wa Ulaya wa kuimarisha mshikamano wake dhidi ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.
Chanzo; Global Publishers