Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy, amesema yuko tayari kuandaa uchaguzi wa urais ndani ya siku 60 hadi 90 endapo hali ya usalama na masharti ya kisheria yatatimizwa, akitoa wito kwa Marekani na washirika wa Ulaya kusaidia kuandaa mazingira salama kwa uchaguzi huo wakati wa vita.
Akizungumza na Waandishi wa habari Desemba 9, 2025 akiwa njiani kuelekea Poland akitokea Roma, Zelenskyy amesema Marekani inataka Ukraine iwe na ahadi za kiusalama ambapo amesema ili hayo yawezekane, Ukraine inahitaji silaha.
Amesisitiza kuwa baadhi ya Wanachama wa NATO bado wana wasiwasi kuhusu uanachama wa Ukraine.
"Tunataka kwa dhati kujiunga na NATO na hilo ni jambo la haki. Lakini tunajua wazi kwamba si Marekani wala baadhi ya nchi nyingine, bado hazioni Ukraine kuwa sehemu ya muungano huo. Na bila shaka, Urusi haitatukubali kamwe, " amesema Zelensky.
Zelenskyy amesisitiza kuwa maamuzi kuhusu kuandaa uchaguzi ni ya Waukraine pekee, akibainisha kuwa suala hilo halikujadiliwa katika mawasiliano yake ya hivi karibuni na maafisa wa Marekani, licha ya Rais wa Marekani Donald Trump, kutoa maoni hadharani kuhusu jambo hilo.
Trump alisema awali kuwa ni wakati wa Ukraine kuandaa uchaguzi, akidai kuwa Kyiv inatumia vita kama sababu ya kutoandaa uchaguzi. Alionya kuwa kukosekana kwa uchaguzi kwa muda mrefu kunaweza kuhatarisha demokrasia ya Ukraine.
Hata hivyo, Zelenskyy alikataa madai kwamba Kyiv inajiepusha na uchaguzi kwa faida za kisiasa, akisisitiza kuwa kuendelea kwa vita hakuhusiani na nani atakayeshikilia madaraka.
Chanzo; Global Publishers