Siku moja tu baada ya kutangaza makubaliano ya kusitisha mapigano na wanamgambo wa Kikurdi wanaoungwa mkono na Marekani, SDF, serikali ya Syria imesema kiasi cha wafungwa 120 wa kundi lijiitalo Dola la Kiislamu, IS, wametoroka gereza la Shaddadi.
Taarifa iliyotolewa leo na wizara ya mambo ya ndani ya Syria ilitangukliwa na ile ya msemaji wa wanamgambo wa SDF, Farhad Shami, aliyesema kwamba waliotoroka walikuwa wapiganaji 1,500 wa IS.
Kwa mujibu wa vyanzo ndani ya serikali, tayari jeshi na vikosi maalum vimewapata 81 kati ya wafungwa hao na vinaendelea kuwasaka wengine.
Jeshi la Syria linalilaumu kundi la SDF kwa kuwaachilia kwa makusudi wafungwa hao, ambao walikuwa kwenye jela inayodhibitiwa na kundi hilo, muda mfupi kabla ya kutangazwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya kundi hilo na serikali. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, vikosi vya SDF vilitakiwa kujiondowa kwenye mikoa ya Raqqa na Deir-el-Zour, mikoa miwili yenye wakaazi wengi wenye asili ya Kiarabu na yenye utajiri wa mafuta na maji na ardhi nzuri ya kilimo, kaskazini mashariki mwa Syria.
Chanzo; Dw