Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema Urusi itatwaa maeneo zaidi nchini Ukraine kwa kutumia nguvu iwapo Kyiv na wanasiasa wa Ulaya aliowaita “nguruwe” hawatakubali mapendekezo ya Marekani kuhusu makubaliano ya amani.
Akizungumza katika mkutano wa kila mwaka wa masuala ya ulinzi ya Urusi, Putin alisema nchi yake inapiga hatua katika pande zote za vita na akasisitiza kuwa Urusi itatimiza malengo yake ama kwa njia ya diplomasia au kwa nguvu, kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters.
“Iwapo upande wa pili na waungaji mkono wao wa kigeni watakataa kushiriki mazungumzo ya maana, Urusi itafanikisha ukombozi wa ardhi zake za kihistoria kwa njia ya kijeshi,” alisema.
Utawala wa Rais wa Marekani Donald Trump unaendesha mazungumzo tofauti na Moscow na Kyiv, pamoja na viongozi wa Ulaya, kuhusu mapendekezo ya kumaliza vita nchini Ukraine.
Hata hivyo, hadi sasa hakujapatikana makubaliano.
Kyiv na washirika wake wa Ulaya wana wasiwasi kuhusu madai ya Urusi yanayosisitiza kuyatwaa maeneo ya Ukraine.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky anataka dhamana kubwa zaidi za kiusalama kufuatia uvamizi wa Urusi, ambayo tangu mwaka 2022 imepeleka maelfu ya wanajeshi nchini Ukraine.
Kwa upande wake, Urusi inadai kudhibiti takribani asilimia 19 ya eneo la Ukraine. Maeneo hayo yanajumuisha Rasi ya Crimea, iliyoiteka mwaka 2014, sehemu kubwa ya eneo la mashariki la Donbas, maeneo makubwa ya Kherson na Zaporizhzhia, pamoja na sehemu za mikoa mingine minne ya Ukraine.
Urusi inasisitiza kuwa Crimea, Donbas, Kherson na Zaporizhzhia sasa ni sehemu ya Urusi.
Hata hivyo, Zelensky anasisitiza kuwa Ukraine haitakubali kamwe uvamizi huo, na karibu nchi zote duniani zinazitambua maeneo hayo kama sehemu halali ya Ukraine.
Chanzo; Bongo 5