Waziri Mkuu wa Denmark, Mette Frederiksen, amesema kuwa Ulaya haitakuwa chini ya shinikizo la vitisho vya ushuru vya Rais wa Marekani, Donald Trump, kufuatia matamanio yake ya kununua Greenland.
Trump alitangaza kuwa atapandisha ushuru wa asilimia 10 kwa bidhaa kutoka nchi nane za washirika wa Greenland iwapo wataendelea kupinga mpango wake wa kuchukua eneo hilo. Frederiksen na viongozi wengine wa Ulaya walitoa taarifa ya pamoja wakisisitiza kuwa ushuru huo unahatarisha uhusiano wa Atlantiki na unaweza kusababisha mzozo hatari wa kidiplomasia.
Trump amesisitiza kuwa Greenland ni muhimu kwa usalama wa Marekani na ameeleza kuwa Washington itapata eneo hilo “kwa njia rahisi au ngumu.”
Trump kupitia mtandao wake wa Truth Social, alisema ongezeko hilo la ushuru wa asilimia 10 litaanza Februari 1 kwa bidhaa zote zinazoingia Marekani kutoka Denmark, Ufaransa, Uholanzi, Ujerumani, Finland, Norway, Sweden na Uingereza, na linaweza kupanda hadi 25% mwezi Juni, hadi pale “makubaliano kamili ya kununua Greenland yatakapotimia
Viongozi wa nchi hizo nane wamesisitiza ushirikiano wao kamili na Ufalme wa Denmark na watu wa Greenland, wakisisitiza umuhimu wa kuimarisha usalama wa Arctic kama maslahi ya pamoja ya Nato.
Frederiksen aliandika pia kwenye Facebook: “Tunataka kushirikiana ila hatutafuti mzozo. Ninafurahi kuona ujumbe thabiti kutoka bara lote: Ulaya haitashinikizwa.”
Trump ameonyesha nia ya kununua Greenland kwa sababu eneo hilo lina rasilimali nyingi muhimu, likiwemo madini na mafuta, na pia ni eneo la kimkakati kwa Marekani kwa kuwa linapatikana kati ya Amerika Kaskazini na Arctic, hivyo ni muhimu katika kurekodi na kudhibiti usalama wa anga na kuangalia shughuli za silaha na meli katika kanda ya hiyo.
Chanzo; Global Publishers