Rais Donald Trump ametumia jukwaa la WEF Davos kufufua azma ya Marekani kuipata Greenland, lakini amesisitiza hatatumia nguvu. Lakini viongozi wa NATO wameonya kuwa mkakati wake unaweza kuisambaratisha jumuiya hiyo.
Rais wa Marekani Donald Trump amelitumia Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF) mjini Davos kusisitiza azma yake ya Marekani kudhibiti kisiwa cha Greenland, akisisitiza kuwa hatatumia nguvu kufanikisha lengo hilo.
Akizungumza mbele ya viongozi wa dunia, Trump alisema kuwa ni Marekani pekee yenye uwezo wa kulilinda na kulihakikishia usalama eneo hilo la Denmark, akitoa wito wa kufanyika “mazungumzo ya haraka” kuhusu uwezekano wa kukinunua Greenland.
“Watu walidhani nitatumia nguvu, lakini sihitaji kufanya hivyo. Situmii na sitatumia nguvu,” alisema Trump katika hotuba yake Davos.
Kauli hizo zilitolewa wakati Trump akirejea Davos baada ya miaka sita, hatua iliyofanya uwepo wake kugubika ajenda nzima ya mkutano wa siku tano wa WEF.
Hotuba hiyo, iliyotarajiwa kujikita zaidi kwenye uchumi wa Marekani, iligeuka kuwa jukwaa la mashambulizi ya kisiasa dhidi ya washirika wa Ulaya.
Trump aliwakosoa vikali washirika wa Marekani barani Ulaya, akiwatuhumu kwa “kukosa shukrani, kukosa uaminifu na kufanya makosa ya sera” katika masuala ya mazingira, nishati ya upepo, uhamiaji na jiografia ya kisiasa.
Chanzo; Bongo 5