Rais wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (Ecowas), Omar Touray amesema kwamba Afrika Magharibi iko katika hali ya dharura kutoka na utamaduni wake uliozoeleka sasa kupinduana.
Hayo ameyasema jana Jumanne Desemba 9,2025 alipokuwa akilihutubia Baraza la Usalama la kikanda mjini Abuja nchini Nigeria.
Haijabainika wazi iwapo tangazo la Touray lilikuwa rasmi na kama ni hivyo, lina maana gani kwa vitendo.
Akinukuu mfululizo wa mapinduzi ya kijeshi, majaribio ya mapinduzi na kuongezeka kwa changamoto za kiusalama, amesema:
"Matukio ya wiki chache zilizopita yameonyesha haja kubwa ya kutafakari kwa kina kuhusu mustakabali wa demokrasia yetu na hitaji la dharura la kuwekeza katika usalama wa jumuiya yetu."
Wachambuzi wanasema kwamba tangazo hilo huenda ni jaribio la Ecowas kurejesha uaminifu wake, baada ya kushindwa kutekeleza tishio la kuingilia kijeshi kufuatia mapinduzi ya mwaka 2023 nchini Niger.
“Ecowas inahofia kuwa mapinduzi ya kijeshi yameanza kuwa jambo la kawaida Afrika Magharibi,” amesema Ulf Laessing, ambaye ni mkuu wa mpango wa Sahel katika Taasisi ya Konrad Adenauer.
“Sasa wanajaribu kuonyesha kwamba wako makini.” amesisitiza.
Pia jana Seneti ya Nigeria iliidhinisha ombi la Rais Bola Tinubu la kutuma wanajeshi nchini Benin kufuatia ombi la serikali ya nchi hiyo. Nigeria ilifanya mashambulizi ya anga dhidi ya magari ya kivita wakati wa jaribio la mapinduzi lililotokea Jumapili.
Chanzo; Mwananchi