Katika hatua iliyoibua taswira ya wasiwasi kisiasa nchini Uganda, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini humo (CDF), Jenerali Muhoozi Kainerugaba, ambaye pia ni mtoto wa Rais Yoweri Museveni, ametangaza kupitia mtandao wa X kumsaka kiongozi wa upinzani, Bobi Wine.
Katika taarifa hiyo iliyosambaa na kuzua mjadala mitandaoni leo Jumanne Januari 20, 2026, Muhoozi amempa Bobi Wine saa 48 kuhakikisha anajisalimisha kwa polisi.
Amesema iwapo Bobi Wine hatatimiza agizo hilo, atachukuliwa kuwa ni mhalifu, atatafutwa kwa operesheni za kihalifu.
Aidha, taarifa ya kumhusu Bobi Wine imekuja katika mfululizo wa taarifa nyingi ambazo Mkuu huyo wa Majeshi ya Uganda amekuwa akiziweka kwa nyakati tofauti tangu kumalizika kwa uchaguzi huo, akitaja operesheni za jeshi hilo kwa wahalifu na hatua linazochukua.
“Ninampa saa 48 kamili kujitokeza mbele ya Polisi, asipofanya hivyo tutamchukulia kama mhalifu au mkaidi na tutamkabili ipasavyo,” amesema Muhoozi kwenye ukurasa wake wa X.
Chanzo; Mwananchi