Kampuni ya ByteDance ya China, mmiliki wa TikTok, imesaini makubaliano ya kisheria yanayolazimisha uhamisho wa umiliki wa sehemu kubwa ya biashara yake nchini Marekani kwa wawekezaji wa Marekani na wa kimataifa, kwa mujibu wa taarifa aliyowasilisha kwa wafanyakazi Mkurugenzi Mtendaji wa TikTok, Shou Zi Chew, Alhamisi.
Kwa mujibu wa waraka huo, nusu ya umiliki wa ubia mpya itakuwa chini ya kundi la wawekezaji wanaojumuisha kampuni za Oracle, Silver Lake pamoja na kampuni ya uwekezaji ya MGX yenye makao yake Abu Dhabi.
Makubaliano hayo, yanayotarajiwa kukamilika tarehe 22 Januari, yanatarajiwa kumaliza jitihada za miaka kadhaa za Serikali ya Marekani kulazimisha ByteDance kuiuza TikTok nchini humo kutokana na hofu za usalama wa taifa.
Hatua hiyo inaendana na makubaliano yaliyotangazwa mwezi Septemba, wakati Rais wa Marekani Donald Trump alipoahirisha utekelezaji wa sheria iliyotishia kuipiga marufuku TikTok iwapo isingeuzwa.
Katika waraka huo, TikTok ilisema makubaliano hayo yatawezesha zaidi ya Wamarekani milioni 170 kuendelea kutumia jukwaa hilo na “kugundua fursa zisizo na kikomo kama sehemu ya jumuiya muhimu ya kimataifa.”
Kwa mujibu wa makubaliano hayo, ByteDance itabaki na asilimia 19.9 ya umiliki wa biashara hiyo. Kampuni za Oracle, Silver Lake na MGX zitamiliki kila moja asilimia 15, huku asilimia 30.1 zikimilikiwa na washirika wa wawekezaji wa sasa wa ByteDance.
Awali, Ikulu ya Marekani ilieleza kuwa Oracle, kampuni iliyoanzishwa kwa ushirikiano na Larry Ellison ambaye ni mfuasi wa Trump, itapewa leseni ya kutumia mfumo wa algorithimu ya mapendekezo ya TikTok kama sehemu ya makubaliano hayo.
Makubaliano hayo yanakuja baada ya ucheleweshaji kadhaa. Mwezi Aprili 2024, wakati wa utawala wa Rais wa zamani Joe Biden, Bunge la Marekani lilipitisha sheria ya kuipiga marufuku TikTok kwa misingi ya usalama wa taifa isipokuwa ikiwa ingeuzwa. Sheria hiyo ilitarajiwa kuanza kutumika Januari 20, 2025, lakini iliahirishwa mara kadhaa na Trump wakati serikali yake ikiendelea na majadiliano ya uhamisho wa umiliki.
Chanzo; Bongo 5