Wizara ya Fedha ya Marekani imewawekea vikwazo ndugu watatu wa Rais wa Venezuela Nicolas Maduro pamoja na makampuni sita yanayosafirisha mafuta kutoka taifa hilo la Amerika ya Kusini.
Taarifa ya Waziri wa Fedha Scott Bessent imesema waliowekewa vikwazo ni wapwa watatu wa mke wa Maduro, Cilia Flores, akidai kuwa wawili kati yao ni "walanguzi wa dawa za kulevya wanaofanya shughuli zao ndani ya Venezuela." Taarifa hiyo imeongeza kuwa Maduro na aliowataja kuwa "washirika wake wa uhalifu" wameingiza dawa nyingi za kulevya Marekani ambazo ni sumu kwa raia.
Washington imechukua hatua hiyo, huku Ikulu ya White House ikisema itaifikisha Marekani meli ya mafuta iliyokamatwa na vikosi vyake hivi karibuni nje kidogo ya pwani ya Venezuela. Hayo yanajiri wakati kukiwa na hofu ya mzozo unaoendelea kufukuta kati ya nchi hizo mbili.
Chanzo; Dw