Kikosi cha 4 cha ulinzi wa amani kutoka Tanzania, ambacho kilikuwa kikihudumu chini ya mwamvuli wa FIB–MONUSCO, kimehitimisha rasmi jukumu lake la ulinzi wa amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Hatua hiyo imeadhimishwa kupitia gwaride maalumu la makabidhiano kati ya TanzQRF ya 4 na TanzQRF ya 5, lililofanyika katika makao makuu ya kambi yao iliyopo mjini Beni–Mavivi, katika Jimbo la Kivu Kaskazini.
Akizungumza mara baada ya gwaride hilo, Kamanda wa Kikosi cha 5, Luteni Kanali David Nkungu, alisema kuwa wanakwenda kutekeleza majukumu yao ya kulinda amani kwa uadilifu na weledi mkubwa.
Kwa upande wake, Meja Rafaeli Ngombale, ambaye alitoa hotuba kwa niaba ya Kamanda wa Kikosi cha 4, Luteni Kanali Omary Yahya aliyemaliza muda wake, alieleza kwamba miongoni mwa mafanikio makubwa ya kikosi hicho ni kurejesha hali ya amani na utulivu katika maeneo yao ya operesheni.
Alisema kuwa kwa sasa raia wanaendelea na shughuli zao za kila siku tofauti na hali ilivyokuwa awali.
Safari ya ulinzi wa amani kwa walinda amani wa TanzQRF Kikosi cha 4 katika Jimbo la Kivu Kaskazini sasa imefikia tamati, na jukumu hilo limekabidhiwa rasmi kwa TanzQRF Kikosi cha 5 kutoka Tanzania.
Chanzo; Bongo 5