Mkuu wa mitihani nchini Korea, Oh Seung-geol amejiuzulu baada ya kutunga mtihani mgumu kupita kiasi.
Mtihani huo ni wa Kingereza wa kujiunga na chuo kikuu nchini Korea Kusini, unaojulikana kama Suneung, ambao umekuwa ukiogopwa, huku baadhi ya wanafunzi wakilinganisha ugumu wake na kusoma maandishi ya kale, na wengine wakiuita 'wazimu'.
Ukosoaji dhidi ya mtihani wa mwaka huu ulikuwa mkali kiasi kwamba ofisa mkuu aliyesimamia mtihani huo alijiuzulu, akilaumiwa kwa mkanganyiko uliotokea.
“Tunakubali kwa dhati ukosoaji kwamba ugumu wa maswali haukuwa sahihi,” alisema mkuu wa Suneung, Oh Seung-geol, akiongeza kuwa mtihani huo “haukutimiza vigezo” licha ya kupitia hatua kadhaa za uhakiki.
Miongoni mwa maswali yaliyowatatiza zaidi wanafunzi ni lile lililohusu falsafa ya sheria ya Immanuel Kant na jingine lililohusisha istilahi za michezo ya mtandaoni.
Chanzo; Nipashe