Maafisa wa Afrika Kusini wamewakamata raia saba wa Kenya wanaotuhumiwa kufanya kazi bila kuwa na nyaraka sahihi za ajira. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Afrika Kusini imesema Wakenya hao walikuwa wakijihusisha na kazi katika mpango wa serikali ya Marekani wa kuwapokea Wazungu wa Afrika Kusini, Afrikaner kama wakimbizi.
Kwa mujibu wa wizara hiyo, uvamizi ulifanyika Jumanne katika kituo cha kushughulikia maombi ya wakimbizi, ambapo raia hao saba wa Kenya walibainika wakifanya kazi huku wakiwa na visa za utalii pekee, jambo linalokiuka wazi masharti yao ya kuingia nchini humo.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa Wakenya hao walikamatwa na kupewa amri za kufukuzwa nchini, na watapigwa marufuku ya kuingia Afrika Kusini tena kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Chanzo; Dw