Rais wa Urusi, Vladimir Putin amesema Urusi itatwaa maeneo zaidi nchini Ukraine kwa kutumia nguvu iwapo Kyiv na wanasiasa wa Ulaya aliowaita 'nguruwe' hawatakubali mapendekezo ya Marekani kuhusu makubaliano ya amani.
Akizungumza katika mkutano wa kila mwaka wa masuala ya ulinzi ya Urusi, Putin alisema nchi yake inapiga hatua katika pande zote za vita na akasisitiza kuwa Urusi itatimiza malengo yake ama kwa njia ya diplomasia au kwa nguvu, kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters.
"Iwapo upande wa pili na waungaji mkono wao wa kigeni watakataa kushiriki mazungumzo ya maana, Urusi itafanikisha ukombozi wa ardhi zake za kihistoria kwa njia ya kijeshi," alisema.
Utawala wa Rais wa Marekani Donald Trump unaendesha mazungumzo tofauti na Moscow na Kyiv, pamoja na viongozi wa Ulaya, kuhusu mapendekezo ya kumaliza vita nchini Ukraine. Hata hivyo, hadi sasa hakujapatikana makubaliano.
Chanzo; Nipashe