Familia ya shujaa wa uhuru wa DR Congo, Patrice Lumumba, imesema imeanzisha upya ufuatiliaji kuhusu ukweli wa kifo cha mwanamapinduzi huyo ambaye alikuwa kipenzi cha Wacongo ili haki ipatikane.
Mahakama ya Ubelgiji imeelezea hatua hiyo ikisema inatafakari uwezekano wa kumshtaki mshukiwa pekee aliyebakia kuhusiana na mauaji ya Lumumba yaliyotokea Januari 17, 1961.
Mjuu wa marehemu waziri mkuu wa zamani wa Congo, Yema Lumumba (33), ameieleza AFP jana Jumanne, alipokuwa akizungumza akiwa nje ya mahakama ya Brussels kabla ya kikao kilichofanyika kwa faragha.
Mtandao wa African News umeeleza kuwa, kwa takribani miaka 15 familia ya Lumumba wamekuwa wakishinikiza kupatikana kwa haki ya kisheria wanayosema imechelewa kwa muda mrefu, kuhusu ushiriki wa maofisa wa Ubelgiji katika mauaji hayo.
“Hatuwezi kurudisha wakati nyuma…lakini tunategemea mfumo wa haki wa Ubelgiji utekeleze wajibu wake na kutoa mwanga ili ukweli ujulikane,” amesema Yema.
Imeelezwa kwamba takribani miaka 65 baada ya Lumumba kunyongwa na mwili wake kuyeyushwa kwa tindikali na wanamgambo wa wa upinzani wakishirikia na mamluki kutoka kwa taifa la zamani la kikoloni, Ubelgiji, Ofisa mmoja wa zamani ndiye aliyesalia hai kukabiliwa na haki.
Chanzo; Mwananchi